Nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappé, amemjibu kwa ukali seneta wa Paraguay, Celeste Amarilla, kufuatia matamshi yaliyoelezwa kuwa ya kibaguzi dhidi yake baada ya ushindi wa Ufaransa wa bao 1-0 dhidi ya Paraguay katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia.
Mbappé aliifungia Ufaransa bao pekee la ushindi kwa njia ya mkwaju wa penalti, matokeo yaliyoiwezesha timu hiyo kutinga hatua inayofuata huku Paraguay ikiondolewa kwenye mashindano. Hata hivyo, baada ya mchezo kumalizika, mjadala uligeukia kauli za Amarilla aliyemshambulia nyota huyo kupitia mitandao ya kijamii kwa matamshi yaliyotafsiriwa kuwa ya kibaguzi na ya kudhalilisha asili yake.
Akijibu tuhuma hizo, Mbappé alimwelezea seneta huyo kuwa ni “mwanamke wa kudharaulika” na kusisitiza kuwa hastahili kushika nafasi ya uwakilishi ndani ya Bunge la Paraguay. Nahodha huyo alisema matamshi hayo yameharibu taswira ya safari nzuri ya timu ya Paraguay kwenye michuano hiyo, badala ya dunia kuzungumzia juhudi na kiwango walichoonyesha wachezaji wao uwanjani.

Kwa upande wake, French Football Federation (FFF) imetangaza kuwa itachukua hatua za kisheria dhidi ya Amarilla. Shirikisho hilo limesema kauli hizo si maoni ya kisiasa pekee, bali ni matamshi ya chuki yanayoweza kuangukia katika makosa ya jinai kwa kuwa yalilenga mchezaji kutokana na asili na rangi yake.
Serikali ya Paraguay nayo imejitenga na kauli hizo, ikisisitiza kuwa haziwakilishi msimamo rasmi wa taifa hilo wala maadili ya wananchi wake. Viongozi wa nchi hiyo wameeleza kuwa wanathamini heshima, usawa na mshikamano katika michezo, licha ya timu yao kuondolewa kwenye mashindano.

Leave a Reply