TRUMP ABADILI SHERIA ZA GREEN CARD

TRUMP AWEKA MASHARTI MAPYA YA UHAMIAJI

Utawala wa Rais Donald Trump umetangaza mabadiliko makubwa katika mfumo wa uhamiaji nchini Marekani, ambapo waombaji wengi wa Green Card sasa watalazimika kurejea katika nchi zao kuwasilisha maombi yao kupitia balozi za Marekani badala ya kufanya mchakato huo wakiwa ndani ya Marekani kama ilivyokuwa hapo awali.

Kwa mujibu wa sera hiyo mpya, wageni wengi wakiwemo wafanyakazi wa teknolojia pamoja na wenzi wa raia wa Marekani watalazimika kuthibitisha kuwa wana “mazingira ya kipekee” ili kuruhusiwa kuomba Green Card wakiwa Marekani. Wasipofanikiwa kufanya hivyo, watahitajika kusafiri nje ya nchi jambo ambalo linaweza kuwaweka katika hatari ya kupoteza hadhi yao ya kisheria pamoja na kushindwa kurejea Marekani.

Maafisa wa idara ya USCIS wamesema hatua hiyo inalenga kurejesha mfumo wa uhamiaji kufuata sheria zilizokusudiwa na kupunguza mianya inayotumiwa na wahamiaji kubaki nchini humo kwa muda mrefu.

Aidha, sera hiyo mpya inatajwa pia kuathiri waajiri wa Marekani wanaotegemea wafanyakazi wa kigeni kupitia visa kama H-1B, huku ucheleweshaji wa maombi katika balozi za Marekani ukitarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na msongamano wa waombaji.

Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Trump wa kuimarisha udhibiti wa uhamiaji nchini Marekani, hasa kuelekea masuala ya uraia wa kuzaliwa pamoja na utoaji wa vibali vya kudumu vya ukaazi.

Wachambuzi wa sheria za uhamiaji wanaonya kuwa sera hiyo inaweza kusababisha familia kutengana kwa muda mrefu pamoja na kuathiri kampuni zinazotegemea wafanyakazi wa kimataifa wenye ujuzi maalum. Pia kuna hofu kuwa waombaji watakaokataliwa visa nje ya Marekani hawatakuwa na nafasi kubwa ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi hayo.

Aidha, mawakili wa uhamiaji wanatarajia ongezeko kubwa la kesi mahakamani kupinga utekelezaji wa sera hiyo mpya, wakieleza kuwa sheria za zamani zilikuwa zinawaruhusu waombaji kuendelea kuishi na kufanya kazi Marekani huku wakisubiri majibu ya maombi yao.

Subscribe YouTube channel

Discover more from OMRIAMA

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading